Share news tips with us here at Hivisasa

Baada ya habari kuenezwa katika kaunti ya Nyamira kuwa lango mpya la kuingia katika Hospitali ya Nyamira level four lilijengwa kwa shillingi millioni saba, afisa mkuu wa afya katika kaunti ya Nyamira Douglas Bosire amejitokeza wazi na kukanusha madai hayo ya utumizi mbaya wa pesa.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano katika hospitali hiyo ya Nyamira level four iliyoko mjini Nyamira, afisa huyo Bosire alikiri kuwa pesa hizo millioni saba zilitumika kwa kujenga lango, nyua, kukarabati hospitali, kupaka rangi ndani na nje ya majengo ya hospitali hiyo pamoja na kujenga mahala pa wagonjwa kukaa ili kusubiri kuhudumiwa.

Kulingana na afisa huyo, serikali ya Kaunti ya Nyamira imenunua mashine nyingi ambazo zimegharimu serikali pesa nyingi ambazo zinahitajika kulindwa kikamilifu ili zisiibiwe, jambo ambalo lililazimu serikali hiyo kujenga lango la kifahari.

“Mashine nyingi zimenunuliwa na serikali ya Kaunti ya Nyamira na mashine hizo zinahitaji kulidwa ndio maana lango likajengwa na majengo ya hospitali yakakarabatiwa kikamilifu,” alisema Bosire.

Aliongezea, “Haya mengine ya kueneza habari kuwa lango liligharimu shillingi million saba ni uwongo kwani pesa hizo zilitumika kwa vitu vingi katika hospitali hii ya Nyamira.”

Afisa huyo wa afya alisema yeyote anayelalamika ama yuko na swali lolote kuhusu ujenzi wa lango anahitajika kuandika barua na kuwasilisha kwa ofisi za kaunti ili aitwe na kuelezewa bayana badala ya kufuata yale ambayo yanaenezwa na watu wasiojua ukweli halisi wa mambo.