Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 72 aliuawa na watu wasiojulikana siku ya Jumapili katika kijiji cha Bocharia, Wilayani Masaba Kaskazini.
Akithibitisha kisa hicho, chifu wa kata ya Keroka Township Kennedy Ndege alisema kuwa genge la watu watatu waliojihami na silaha butu walivamia boma ya marehemu, Teresa Kwamboka, anayeishi na mjukuu wake.
Chifu huyo alielezea kuwa majambazi hao walitaka kupewa pesa lakini Kwamboka aliposema kuwa hana pesa, wezi hao walimgeukia na kumkatakata kwa panga hadi kufa na mwishowe wakachukua viti kumi aina ya plastiki na kutokomea.
"Genge la wahalifu watatu walifika kwa marehemu Kwamboka na kubomoa lango kuu na kuingia kwa nyumba walipomkatakata kwa panga,” alisema Ndege.
Ndege alisema kuwa juhudi za majirani waliofika kusaidia ziligonga mwamba kwani washukiwa hao waliwarushia panga walizokuwa nazo na kumumiza mmoja wa majirani hao.
Alisema kuwa maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Gucha mjini Keroka.
"Maafisa wa polisi walifika katika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu na wametuhakikishia kuwa uchunguzi umeanzishwa,” alisema Ndege.