Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwanasiasa wa kike kutoka eneo la Soy amewataka akina mama kujitokeza kwa wingi na kugombea viti vya uwakilishi wadi kama njia moja ya kuhakikisha usawa wa jinsia katika jamii.

Akizungumza huko Soy siku ya Ijumaa, Florence Akumu aliwapa changamoto akina mama kugombea viti vingi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Akumu alisema hiyo itakuwa njia moja ya kuhakikisha kuwa akina mama wana jukumu katika jamii ikiwemo kuunda sheria za kaunti.

Alisema akina mama lazima wawe msitari wa mbele kupigania haki zao za kikatiba.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mwakilishi wadi mteule wa chama cha KANU katika Kaunti ya Kakamega Sellah Keya, aliyesema kuwa akina mama ambao wanaonyesha ari na tamaa ya kugombea viti tofauti tofauti vya kisiasa ni wachache mno jambo ambalo linachangia wanaume wengi kunyakua viti hivyo.

"Sisi kina mama hatuwanii viti halafu wanaume wakishinda na kuanza kutunyanyasa tunaanza kulalamika,” alisema Keya.

Kuhusu suala la mgomo wa walimu, Akumu aliisuta serikali ya kitaifa kwa kile alichokitaja kama utepetevu kazini.

"Watoto wetu wako nyumbani wanahangaika huku watoto wao wakiendelea na masomo katika shule za kibinafsi,” alisema Akumu.

Aliitaka serikali ya kitaifa kuingilia kati mara moja na kutatua suala hilo la mgomo wa walimu.

"Ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa wafanyikazi wake wanalipwa mishahara inayofaa tena kwa wakati unaofaa ili kuzuia visa kama hivi kutokea,” alisema Akumu.