Baraza la Magavana limeshikilia kwamba lazima serikali iwalipe walimu nyongeza yao wanayodai ya asilimia 50 hadi 60 ili kusitisha mgomo wa walimu uliyoingia wiki yake ya nne.
Kulingana na Naibu Mwenyekiti wa Baraza hilo Salim Mvurya, hatua ya serikali kudinda kuwalipa walimu ni kinyume na katiba ya nchi pamoja na ukiukaji wa haki za watoto.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Mvurya alisema kwamba wanachama wa baraza hilo watalishinikiza bunge la seneti kupitisha mswada bungeni wa kumbandua mamlakani waziri wa elimu Jacob Kaimenyi kwa kukosa kuliwajibia swala la walimu jinsi ipaswavyo.
“Serikali inakiuka haki za watoto na katiba ya nchi. Tungependela serikali iwalipe walimu nyongeza wanayodai ya asilimia 50 hadi 60 na iwapo haita fanya hivyo, basi tutalishinikiza bunge la seneti kuchukua jukumu,” alisema Mvurya.
Gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Joho alisema kwamba hatua ya Rais Uhuru Kenyatta ya kusema kuwa serikali haina fedha za kuwalipa walimu imekaidi katiba ya nchi na kumtaka rais kutii agizo la mahakama.
Aidha, alipendekeza kuwepo kwa vikao vya mazungumzo baina ya Tume ya kuratibu mishahara ya wafanyikazi wa umma, Tume ya kuajiri walimu pamoja na vyama vya kutetea maslahi ya walimu nchini Knut na Kuppet, ili kuutatua mgogoro huo.
Haya yamejiri baada ya Rais Uhuru Kenyatta kusema kuwa serikali haina pesa za kuwalipa walimu.