Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Viongozi wa baraza la Maimam na wahubiri kutoka kanda ya North Rift wamepedekeza kuondolewa kwa marupurupu ambayo wanasiasa hupewa.

Wakizungumza siku ya Jumapili, viongozi hao walisema kuwa wanasiasa wanapoomba kura wao husema wanataka kuhudumia wananchi hivyo basi hawapaswi 'kunyonya' wananchi kupitia kwa marupurupu wanayopata.

Mwenyekiti wa baraza hilo Sheikh Abubakar Bin alisema marupurupu mengine ambayo wanasiasa hupewa huongezea wananchi mzigo wa ushuru.

Sheikh Bin alisema tabia ya wabunge, maseneta, magavana miongoni mwa wanasiasa wa matabaka mbalimbali kupewa marupurupu mengi ndio hufanya wafanyikazi wengine kulipwa mishahara duni.

Sheikh Bin alisema marupurupu hayo huchangia katika ufisadi huku wananchi wa matabaka ya chini wakiendelea kuzama katika umaskini.

“Wanasiasa wanataka kupokea marupurupu ya kila aina bila kujali walipa ushuru husika. Tabia hii ndio tunataka tukomeshe na hata kupunguza udadi ya wabunge,” alisema Bin.

Sheikh Bin alipendekeza kutupiliwa mbali kwa kiti cha wakilishi wa wanawake katika kaunti huku akisema kuwa haoni manufaa ya kiti hicho.

Akirejelea hoja ya mbunge wa Budalangi Ababu Namwamba ya kutaka mishahara ya wanasiasa na maafisa wakuu serikalini kupunguzwa, Sheikh Bin alitaka wabunge kuunga mkono hoja hiyo iwapo wanajali maslahi ya Wakenya wote.