Share news tips with us here at Hivisasa

Kati ya asilimia 18 na 30 ya watumizi wa dawa ya kulevya katika ya Mombasa wameathirika na virusi vya ukimwi.

Hii ni asilimia 5.6 zaidi ya watu waliyoathika na virusi hivyo humu nchini.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Ijumaa katika hospitali kuu ya eneo la Pwani, wakati alipozindua kliniki ya kuwatibu waathiriwa wa dawa za kulevya yaani Medically Assisted Therapy iliyofadhiliwa na shirika la UNODC, Waziri wa Afya katika kaunti ya Mombasa Binti Omar alisema kuwa mradi huo utasaidia pakubwa.

Binti alisema kwamba kliniki hiyo itatoa matibabu maalum kwa waathiri hao pamoja na dawa ya kupunguza makali ya utumizi wa mihadarati aina ya methadone ili kuona kwamba vijana waliyojitosa katika janga hilo wananusurika.

“Tumezindua mradi huo uliyofadhiliwa na UNODC kuwasadia vijana wetu waliyoathirika na virusi vya ukimwi kutokana na wao kutumia mihadarati. Hatua hii itasadia pakubwa kupunguza idadi ya vijana kutumia dawa za kulevya,” alisema Binti.

Kulingana na waziri huyo, kliniki hiyo inalenga kutoa huduma kwa waathirika wote wa kike na wakiume haswa wanaotumia mihadarati aina ya heroine hali ambayo inatarajiwa kubadilisha tabia ya waathiriwa hao ili kuzisadia jamii zao.

“Kwa sasa tutakuwa tunawahudumia wale wanajidunga sindano wakitumia uraibu wa heroni ili kuwasadia kujinasua katika utumizi wa mihadarati. Tungependa kuwaomba watu wote wataongia kwa huu mradi lazima wajihusishe kikamilifu ili tuweze kuwasadia,” aliongeza Binti.

Waziri huyo wa afya wa kaunti ya Mombasa amewashinikiza wakaazi kuwashauri vyema vijana waliyojitosa katika jinamizi hilo kujitokeza na kupata matibabu maalum na kuachana na utumizi huo wa dawa zakulevya.

Hata hivyo ameitaka jamii kushiriki ipasavyo katika kufanikisha mradi huo kwani kliniki hiyo inauwezo wa kuhudumia waathiriwa zaidi ya 600.