Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wabunge wametakiwa kujadili miswada inayoambatana na katiba na wala sio kuhitilafiana na mapendekezo yaliyo kwenye katiba.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, afisa mkuu wa kituo kinachoangazia mfumo wa demokrasia ya vyama vingi cha ‘Centre for MultiParty Democracy’ Lina Mkasi, alisema kwamba katika siku za hivi majuzi, wabunge wameonekana kuibuka na miswada inayopingana na katiba na wanapaswa kukoma.

Kulingana na Mkasi, kucheleweshwa kwa miswada inayopigania usawa wa kijinsia ni swala ambalo bunge hilo limefanya kwa kusudi bila ya kufahamu kwamba miswada hiyo ina umuhimu mkubwa kwa demokrasia ya nchi.

Mkasi alisema kwamba miswada isiyofaa kama ule unaolenga kuwakandamiza wanahabari ni mambo ambayo kamwe hayafai kujadiliwa bungeni, huku akishikilia kwamba wabunge katika bunge la Kitaifa wanastahili kuwajibikia majukumu yao kikamilifu.

"Tunasikitishwa na baadhi ya wabunge kujadili miswada isiyokuwa na umihimu wowote wala kumfaidi Mkenya. Kuna maswala muhimu yanayofaa kujadiliwa bungeni na kuimarisha malengo ya wananchi mashinani lakini bunge limekosa mwelekeo na kuvuruga vipengele muhimu vya katiba. Hilo tunataka lisitishwe mara moja,” alisema Mkasi.

Tayari miswada iliyopaswa kupitishwa mwezi Agosti mwaka huu iliahirishwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kutoa nafasi kwa wabunge hao kujadiliana kuhusu maswala tata kwenye miswada hiyo ukiwemo ule wa usawa wa jinsia.