Chuo Kikuu cha Technical University of Mombasa kimefungwa kwa muda usiyojulikana baada ya wanafunzi kugoma wakilalamikia nyongeza ya karo.
Kulingana na wanafunzi hao, chuo hicho kimeongeza karo ya shule kwa Sh5,000 hadi Sh6,000 zaidi bila ya kutoa maelezo yoyote kuhusiana na kile kilichopelekea nyongeza hiyo.
Wanafunzi hao walikongamana chuoni humo siku ya Jumatatu na kuanza kuimba nyimbo za kupinga nyongeza hiyo ya karo na kuyateketeza magari mawili ya kubeba taka ya Serikali ya Kaunti ya Mombasa.
Hali hiyo ililazimu usimamizi wa chuo hicho kukifunga chuo hicho na kuwapatia wanafunzi hao muda wa saa moja kukusanya virago vyao na kuondoka mara moja chuoni humo.
Maafisa wa Polisi waliwatia nguvuni wanafunzi kadhaa chuoni humo kufuatia uharibifu wa mali ya chuo hicho na zile za kibinafsi.