Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Bobasi iliyoko Kaunti ya Kisii Stephen Manoti amethibitisha kuwa Hospitali ya Nyamache Level Four imepata fedha ya kujenga chuo cha kutoa mafunzo ya udaktari kutoka kwa CDF.  

Wakazi wa eneo bunge hilo sasa wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kupashwa habari ya kujengwa kwa madarasa na kuanzisha chuo kipya cha kutoa mafunzo ya udaktari kwa wanafunzi wanaosomea taaluma hiyo.

Hospitali hiyo ilikabidhiwa Sh2 milioni kutoka kwa hazina ya ustawi ya maeneo bunge (CDF) ambazo zilitolewa na mbunge wa eneo bunge hilo Manoti.

Akizungunza siku ya Jumamosi katika hafla ya kuchangisha fedha za ujenzi wa Kanisa ya Kiadventista ya Nyantira iliyoko katika eneo bunge lake, Mbunge Manoti alisema waliweza kupata idhini kutoka serikali kuu ya kuanzisha chuo hicho kipya cha kutoa mafunzo ya udaktari.

“Tayari tumeanza kujenga madarasa na tutajenga madarasa mengi ili watoto wetu wapate fursa ya kusomea udaktari hapa kwetu,” alisema Manoti.

Wakati uo huo, Mbunge Manoti alisema kuwa ingawa pesa hizo hazitoshi kwa ujenzi huo hadi ukamilike, serikali kuu itawaongeza Sh2 milioni zingine ili kila kitu kikamilika vile kunavyostahili.

“Naomba wazazi kuwaleta wanao kwanzia mwenzi wa tisa katika chuo hicho kilichoko katika hospitali ya Nyamache ili wapate masomo ya udaktari,” aliongeza Manoti.

Wakazi wa eneo hilo ambao hawangeweza kuficha furaha yao kufuatia kuanzishwa kwa chuo hicho katika hospitali ya Nyamache, walimpongeza Mbunge Manoti kwa kuwapelekea maendeleo hayo.