Chuo kikuu cha Kisii kitaanzisha somo la kutunza mazingira na kuibadilisha taka kuleta mapato badala ya kutupwa kiholela kwenye mitaa.
Hii ni njia mojawapo ya kuiweka kaunti ya Kisii mbele katika masuala ya usafi na mazingira kwa jumla. Shughuli hiyo itasimamiwa na kaunti hiyo kwa ushirikiano na Chuo kikuu cha Kisii.
Haya yalisemwa na Naibu Chansela wa chuo hicho Profesa John Akama katika mkahawa wa kifahari wa Nyakoe viungani mwa mji wa Kisii siku ya Jumanne katika uzinduzi rasmi wa uhifadhi salama na udhibiti wa taka katika kaunti hiyo.
Profesa Akama aliwashauri wageni pamoja na vyombo vya habari kuwa katika mstari wa mbele kutangaza na kuwaambia wakazi umuhimu wa kutunza mazingira katika miji na popote wanapoishi ili kuepusha na kupata maradhi kama ya saratani ambayo mara nyingi hupatikana katika madini fulani.
Profesa huyo alisema mradi huo kwa jumla utahakikisha kuwa vidude vya kielektroniki kama vile simu, pasi, televisheni na vyombo vya habari vinahifadhiwa mahali mbali na makazi na kuletwa katika kituo ambacho kitaanzishwa katika kaunti.
“Tuwajibike kwa kutunza mazingira yetu, na mradi huu unalenga kupunguza taka hasa za kielektroniki zinazoaminika kusababisha madhara kama saratani,” alisema Profesa Akama.