Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mahakama kuu iliyo jijini Mombasa imeagiza upande wa mashtaka kwenye kesi inayohusu mashirika mawili ya kutetea haki za kibinadamu kuharakisha uchunguzi wao la sivyo kesi hio itupiliwe mbali.

Mahakama hiyo imeipa afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashataka ya umaa (DPP) na ile ya mkuu wa sheria siku 14 kuhakikisha zinajitayarisha kikamilifu kwa kesi hiyo inayohusu kufungwa kwa muda kwa akaunti za benki ya shirika la Muhuri na lile la Haki Africa.

Hii ni baada ya maafisa kutoka afisi hizo mbili kuomba muda zaidi ili kujitayarisha kwa kesi hiyo.

Hatua hiyo ya kuongeza muda ilipingwa vikali na wakili kutoka shirika la kitaifa la kutetea wa haki za kibinadamu KNHRC, Victor Kamau.

Wakili huyo aliiambia mahakama kuwa jambo hilo ni ukiukaji wa haki za binadamu na kuitaka mahakama kuharakisha kusikiliza kesi hiyo ili haki ipatikane.

Akaunti za mashirika hayo zilifungwa na serikali baada ya kutuhumiwa kufadhili makundi ya kigaidi nchini, likiwemo kundi lile la al-Shabaab.

Kesi hiyo itasikilizwa Oktoba 2 mwaka huu.