Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi wa Kisii wameiomba idara ya trafiki na wasimamizi wa waendeshaji bodaboda katika Kaunti ya Kisii kuwaambia wanaoendesha bodaboda kuzingatia sheria za barabara.

Hii ni baada ya waendeshaji bodaboda hao kuwabeba wanafunzi wa shule za upili zaidi ya watatu kwa pikipiki moja, jambo ambalo wakazi hao walilikashifu na kusema huenda maisha ya wanafunzi yawe hatarini kwani wanafunzi hao hawaogopi kwa kulipishwa pesa kidogo na waendeshaji bodaboda hao.

Wakizungumza na Mwandishi huyu siku ya Jumatano katika eneo la Marani, wakazi hao ambao wengi wao ni wazazi wakiongozwa na Haroni Osiemo, wameiomba idara ya trafiki pamoja na wasimamizi wa wandeshaji bodaboda katika eneo hilo la Marani kuwachukulia hatua kali za kisheria waendeshaja bodaboda wanaovunja sheria za barabara kwa kuwabeba wanafunzi zaidi ya mmoja.

“Hatuwezi subiri hadi maafa yatokee kupitia ajali za barabara. Heri kinga kuliko tiba. Tunaiomba idara ya trafiki iwachukulie hatua kali za kisheria wanaovunja sheria za barabara,” alisema Judy Moraa, mzazi.

Aidha, wakazi hao wamewaomba wanabodaboda hao kukoma kutumia maneno machafu wanapofanya usafiri wao kwa kutusiana wao wenyewe kwa wenyewe wakisema kuwa wanaaibika sana haswa wanapowasindikiza wanao shuleni, jambo ambalo wameomba lishughulikiwe pia na wasimazi wa waendeshaji bodaboda hao.