Gavana wa Mombasa amesema ukosefu wa msingi bora wa elimu katika jamii umechangia kukithiri kwa maswala ya misimamo mikali miongoni mwa vijana wadogo na kusababisha ukosefu wa usalama nchini.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumanne, Gavana Hassan Ali Joho alisema wazazi wamechangia pakubwa kwa vijana wao kujiunga na uhalifu na kuvuruga usalama wa nchini kutokana na kuzembea katika majukumu yao na kusabanisha elimu duni kwa mtoto.
Joho alisema kwamba kupitia elimu bora hasa kuanzia elimu ya chekechea, basi vijana wengi watafanikiwa kujitenga na baadhi ya watu waliyo na malengo potuvu ya kubadili fikra za vijana na kuwafanya kujiunga na misimamo mikali.
“Vijana wengi wamejiunga na maswala ya misimamo mikali kutokana na ukosefu wa msingi bora wa elimu na elimu hiyo huanzia katika shule za chekechea hadi zile za ngazi ya juu. Iwapo mtoto atakosa msingi huo, basi itakuwa rahisi kwa wahalifu na magaidi kumshawishi na kumsababisha kujiunga na mambo ya mismamo mikali,” alisema Joho.
Gavana Joho amewahimiza wazazi kuzingatia swala la elimu na kuwashinikiza watoto wao kupata msingi bora wa elimu ili kuwaepusha kujiunga na maswala ya kihalifu na ugaidi na kudhibiti usalama.
Aidha, alisema kwamba hakuna dini katika dunia hii inayoruhusu mtu kumtoa mwenzake uhai wala kujihusisha na ugaidi, na kuongezea kuwa dini inamfunza mtu maadili mema na jinsi ya kuishi na wenzake kwa amani.
“Hakuna dini inayoruhusu mtu kumtoa mwenzake uhai wala kujiunga na ugaidi na mimi leo nawaambia muwe watu waadilifu na wenye kupenda kudumisha amani,” alisema Joho.
Gavana joho ameahidi kuimarisha viwango vya elimu katika kunti hiyo kwa kujenga msingi bora wa elimu ya mtoto ili kumwezesha kujimudu katika siku za usoni.