Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti ya Nakuru itatumia Sh4 milioni kujenga bomba jipya la maji taka katika kitongoji cha Bondeni mjini Nakuru kufuatia kuzibika kwa bomba la awali.

Mkurugenzi mkuu wa idara ya maji ya Nakuru Johnson Kamau alisema mjenzi aliyekabidhiwa jukumu la kutekeleza shughuli hiyo tayari yuko katika eneo la kujengwa bomba hilo na ujenzi huo unatarajiwa kuchukua muda wa wiki sita.

Kamau alisema kuwa chanzo kikubwa cha kuzibika kwa bomba la maji taka lililokuwa likitumiwa hapo mwanzoni ni ujenzi duni na watu kutupa taka kiholela kwenye maeneo ya umma na barabara katika sehemu hiyo.

Mkurugenzi Kamau aliongeza kuwa tayari wameshafanya majadiliano na idara ya kusimamia afya ya umma katika kaunti hiyo ili wawape muda zaidi wakamilishe ujenzi huo kabla ya kuchukua hatua zozote za kisheria dhidi ya waliohusika katika uharibifu wa bomba la awali.

Alisema pia wameungana na kampuni ya maji na usafi Nakuru (NAWASSCO) kwenye ujenzi huo unaonuia kutoa huduma bora za kukabiliana na uchafu eneo hilo. Aliongeza kuwa kama idara ya maji, wamejitolea katika utendakazi wao kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

"Tayari tushafanya majadiliano na kitengo cha kusimamia afya ya umma katika Kaunti ya Nakuru ili itupe muda unaohitajika kumaliza shughuli hii muhimu kabla ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waharibifu wa bomba la awali," alisema Kamau.