Kaunti ya Uasin Gishu imetenga kitita cha Sh5m kusaidia wauzaji pombe haramu ambao wamerekebisha tabia.
Fedha hizo zitatumika kusaidia wahusika kuanzisha biashara mbadala ya kujikimu maishani.
Akizungumza siku ya Alhamisi, mkurugenzi wa bodi ya kudhibiti pombe na vileo katika kaunti hiyo Bw Armstrong Rono alisema hatua hiyo ni miongoni mwa mipango ya kaunti hiyo kusaidia waraibu hao kukumbatia biashara mbadala.
Bw Rono alisema idadi kubwa ya waraibu hao walikuwa wakitegemea pombe haramu kujipatia riziki ndiposa kuna haja ya kuwasaidia kujikimu maishani baada ya kauchana na biashara ya pombe haramu.
Bw Rono alisema idara yake itaendeleza mafunzo ya kusimamia biashara kwa walengwa kabla ya kuanza kuwapa pesa hizo kupitia kwa makundi.
“Tumetenga kima cha Sh5m kusaidia waliokuwa wauzaji na wagema wa pombe haramu kuanzisha biashara mbadala baada ya kuachana na biashara hiyo, lakini tutahakikisha kuwa wamepata mafunzo kuhusu biashara kabla ya kuwapa pesa hizo,” alisema Rono.
Bw Rono alitaka waliokuwa wagema na wauzaji wa pombe hiyo kujiunga na makundi ya maendeelo ili kunufaika na fedha hizo.
Wakati huo huo Bw Rono alisema bodi yake imeanzisha msako dhidi ya wazazi ambao huenda katika baa na maeneo ya starehe wakiwa na watoto hasa siku siku za wikendi.
Alisema kwamba watakaoapatikana na watoto katika maeneo hayo watachukuliwa hatua za kisheria.