Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mahakama makuu ya Mombasa yameahirisha kesi ya uchochezi dhidi ya mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Mombasa, Mishi Mboko, baada ya baadhi ya mashahidi ambao walitarajiwa kuwa mbele ya mahakama hayo kukosa kuhudhuria kesi hiyo.

Kesi hiyo iliwasilishwa mbele ya mahakama kuu ya Mombasa na serikali kwa madai kuwa Mboko, alitumia maneno ambayo yana azimio ya uchochezi dhidi ya wananchi mwaka wa 2014 katika siku kuu ya Madaraka mjini Mombasa.

Mwendesha mashtaka kwenye kesi hiyo Nicolas Gitonga, alitaka korti impe muda kutayarisha faili na kujua kilichosababisha mashahidi hao kukosa kufika kortini siku ya Alhamisi kutoa ushahidi wao kuhusiana na kesi hiyo.

Mboko ameaminika kuwa mtetezi mkubwa wa wakazi wa eneo zima la pwani na ni kiongozi wa tatu miongoni mwa viongozi wa mlengo wa upinzani kujipata katika mikono ya sheria dhidi ya uchochezi.

Hata hivyo baadhi ya wakazi kutoka maeneo ya pwani wamemtetea mwakilishi huyo wa wanawake kwa kudai kuwa serikali imeshindwa kuwakabili viongozi kutoka upande wa serikali ambao wamesikika mara nyingi wakitoa maneno yenye hisia za ukabila na zenye chuki zaidi kuliko anachoshtumiwa mwakilishi huyo wa wanawake kutoka Mombasa.

Wakazi hao wameitaka serikali kutotumia njia za kupendelea wanaposhughulikia masuala ya uchochezi hasa yanayowahusisha viongozi wenye nafasi serikali na siasa.