Gavana wa Kaunti ya Nairobi Evans Kidero ameitaka serikali kuwacha kuvunja sheria zilizotungwa mahususi kwenye katiba.
Kidero alidai kuwa serikali kuu inataka kunyanganya serikali za kaunti mamlaka ya kusimamia baadhi ya vitengo muhimu na kutaka wabunge kutunga sheria za kuzipa kaunti nguvu zaidi.
Akiongea katika mazishi ya mbunge wa zamani wa eneo bunge la Kitutu Masaba, Makone Ombese, Kidero alidai kuwa serikali kuu bado inaendelea na mipango yake ya kuvuruga sera za ugatuzi.
Aliitaka serikali ya Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake Bwana William Ruto, kuzingatia na kutekeleza ahadi walizotoa kwa wananchi kuwa watahakikisha kuwa sera zote na sheria zilizotungwa kikatiba hazitabadilishwa kwa njia yoyote ile.
Kidero aliongeza kuwa watafanya kazi na serikali kuu iwapo upande wa serikali utaheshimu maoni ya wakenya na viongozi wengine kwa jumla.
Kidero alisema Bwana Makone alikuwa kiongozi aliyepigania haki za wanyonge na alikuwa mbunge aliyeleta demokrasia ikizingatiwa kuwa mbunge huyo alikuwa miongoni mwa wabunge waliohudumu kwenye mabunge ya awamu ya kwanza na ya pili, baada ya taifa la Kenya kujipatia uhuru kutoka kwenye mikono ya waingereza.
Aliwataka viongozi wote kutoka maeneo yote nchini kuiga mfano wa Makone na wabunge wa zamani ambao walipigania haki za wakenya wote.