Share news tips with us here at Hivisasa

Mwili wa kijana mmoja katika Kijiji cha Mwamosioma, viungani mwa mji wa Kisii ulipatikana umeninginia kwa kamba katika chumba chake Jumapili asubuhi.

Wakazi wanakisia kuwa Benson Matunda alijitoa uhai kutokana na mzozo wa kimapenzi baada ya bibiye kumwacha na kurudi kwao mjini Nakuru.

Kulingana na jirani wa mwenda zake, Winne Atieno, marehemu alitoka kazini siku ya Jumamosi na kuzungumza naye kwa upole huku akimuuliza ikiwa bibinyake alikuwa amerudi. Baada ya mazungumzo kidogo na kuarifiwa kuwa bibi yake hakuwa amerudi Matunda aliingia chumbani mwake na hakutoka tena.

“Alikuja jana usiku akanisalimia kama kawaida na kuniulizia kama mke wake amerudi na nikamwambia bado hajaonekana kwenye ploti, yeye aliingia na kulala kama kawaida lakini asubuhi tulisikia akiitwa na rafiki yake wanayefanya naye kazi mjini pale Coko Beach Hotel," alisema.

Atieno alisema kuwa alijaribu kumwita baadaye lakini hakupata jibu ndipo ikambidi kuchungulia.

"Rafiki yake alipokwenda, nasi baadaye tulijaribu kumwita lakini hakujibu. Ikanibidi nichungulia kwenye tundu dirishani nikaona amejifunga kitu kama nguo shingoni nikaita majirani,” alisema jirani.

Aidha jirani mwingine, Eric Mogirango, ambaye walifanya kazi naye kwenye hoteli hiyo iliyoko mjini Kisii alisema kuwa kijana huyo alikuwa na mzozo na bibi yake, baada ya kumwambia kuwa anaenda kujiunga na chuo jambo analosema anashuku halikumfurahisha marehemu.

Kiongozi mmoja katika kijiji hicho, Charles Ogwang' alipiga ripoti kwa polisi ili wachunguze kisa hicho na kupeleka mwili wa marehemu katika chumba cha kuifadhi maiti.  Polisi hawakuwa wamewasili kabla ya kuandika taarifa hii. 

Inasemekana marehemu ameishi kwenye nyumba hiyo kwa miezi tisa baada ya kuhamia huko kutoka Kebirigo, Nyabara Ibere kaunti ya Nyamira.