Kijana mmoja kutoka Tabaka, Kaunti ya Kisii anaendelea kuvuna vinono kutokana na kipaji cha kuchonga na kutengeneza bidhaa mbali mbali kutoka kwa vinyago.
Huku maonyesho ya kilimo katika eneo la Gusii yakiendele, kijana Paul Magori ambaye amekuwa katika kazi hiyo ya kuchonga vinyago kwa zaidi ya miaka 10 alisema amekuwa akiuza bidhaa zake kwa watalii kila mara na baadhi ya wenyeji.
Hata hivyo, Magori alisema watu wa hapa Kenya wana tabia ya kupuuza na kumkejeli wanaponunua vitu vyake ambapo aliwataka kujivunia kilicho chetu.
Magori ambaye aliacha shule baada ya mtihani wa darasa la nane aliwashauri vijana kufuata ndoto yao huku akisema kuwa vipawa hupewa na Mungu hivyo sharti vitumiwe vilivvyo.
Licha ya kisomo chake kidogo, kijana huyo alisema kuwa amefanikiwa kutembelea mataifa mengi ya Afrika Mashariki, ikiwemo Rwanda, Tanzania na Uganda huku akifanikiwa kuuza zaidi ya Sh50,000 kwa kila kinyago anachosafirisha kwenda nje.
Aliwasihi vijana kutumia nafasi hio ya maonyesho na kujifundisha mambo mseto yakiwemo ya kilimo na jinsi ya kukifanya pia na kutembelea kila kibanda ndani ya uwanja ili kupata ujuzi kutoka kwa wenzao.
Aliomba serikali ya Kaunti ya Kisii kuanza kuwafadhili vijana kifedha ili kujiendeleza katika vipaji na kujiinua kimapato na kuahidi kuwa atafanya kila awezalo kutangaza Kaunti ya Kisii nje ili kuleta watalii katika kaunti hiyo kujionea masuala ya uchongaji.