Kikao katika Bunge la Kauti ya Kisii kilikosa kuendelea siku ya leo na kuhairishwa hadi kesho (Ijumaa) baada ya Wawakilishi wa Wadi kukosa kuafikia kikao cha leo kwa madai ya kutolipwa.
Wawakilishi hawo wanadai kuwa hawajalipwa marupu rupu yao ya kamati za bunge hilo ilhali kamati hizo zimekuwa na vikao mara kwa mara.
Kinara wa bunge hilo Kerosi Ondieki aidha alilazimika kuchukua hatua hiyo ya kuhairisha kikao cha leo hadi siku ya kesho baada ya Wawakilishi wanne pekee kuafikia kikao cha siku ya leo.
Ondieki alisema kuwa lilikuwa ni jambo la kushtua sana kuona kuwa bunge nzima lilikuwa na Wawakilishi wanne pekee na kwa hiyo lolote halingeweza kuendelea katika bunge, ila kuhairisha kikao hadi siku iliyofuata ambapo Wawakilishi hao watatumiwa ujumbe wa kuwaarifu maendeleo yatakayofanyika.
"Ni jambo la kushangaza kukosa Wawakilishi katika jumba bila kupata mawasiliano yoyote na kwa hiyo sina budi ila kuhairisha kikao hadi kesho,” alisema Ondieki.
Kaunti hiyo ya Kisii ina Wawakilishi sabini na mmoja wakiwemo wale walioteuliwa kuwakilisha makundi maalum na wanasemekana kutoridhika na kuchelewa kulipwa marupu rupu yao ya vikao katika kamati za bunge hilo.
Haya yanajiri tu baada ya ripoti maalum kuhusu bunge hilo kuonyesha kuwa walitumia pesa nyingi kupita kiasi kama bunge la Kaunti ya Kisii.