Shirika moja lisilo la kiserikali, The Broad Kenya, kutoka Kaunti ya Kisii, linalenga kuwafadhili vikundi vya kina mama wajane ili waweze kujiendeleza katika maisha yao.
Afisa mkuu wa shirika hilo ambalo limekuwa likiwafadhili wajane wa zaidi ya miaka 65 katika baadhi ya maeneo ya Kisii, alisema kuwa wanalenga kuwafikia wajane wote katika kila eneo bunge kwenye kaunti hiyo.
Akiongea siku ya Jumanne katika eneo la Nyambene, divisheni ya Nyamarambe katika eneo bunge la Mugirango Kusini, wakati wa kuwakabidhi wajane hao mablanketi, afisa huyo Bi Josphine Bonareri aliwashauri kina mama ambao bado hawajafikisha umri wa miaka 65, kujiweka katika vikundi ili wapokezwe mikopo ya kujiendeleza katika maisha.
"Kina mama wanastahili kujiunga na vikundi mbalimbali za kujadili masuala ambayo yatawafaa kimawazo na kuifaa jamii kwa jumla na kujiepusha kukaa pekee kwasababu hali hiyo huwafanya wengine kuzeeka haraka kwa kuwa na upweke mkubwa," alisema Bonareri.
Afisa huyo pia aliwasihi viongozi wote kutoka Kaunti ya Kisii kushikana mikono ili kuwatafutia njia za kifedha na kuwafadhili kina mama kama njia moja ya kuinuia na kuboresha uchumi hasa wa wajane ambao mara nyingi huwa na taabu pindi wanaume zao wanapoaga dunia na kupata mzigo mkubwa wa kulea watoto wao.