Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwenyekiti wa chama cha kutetea haki ya walimu (KNUT) tawi la Nyamira Kennedy Nyamwanda amelalamikia vikali tume ya kuajiri walimu nchini (TSC) kwa kuwahamisha walimu katikati mwa muhula bila kuangalia mahitaji yao.

Akizungumza na Waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika mji wa Nyamira, mwenyekiti Nyamwanda alisema kuwa uamuzi wa tume ya TSC sio halali kwa kuwahamisha walimu hadi shule zingine katikati mwa muhula wakati wengine wana somo la kuwafundisha wanafunzi ambalo tayari hawejakamilisha na kusema hiyo itachangia wanafunzi kufanya vibaya katika mtihani wa kitaifa.

"TSC limekosea kwa kuwahamisha walimu bila kuhusisha chama cha KNUT,  haswa katikati mwa muhula. Huo sio uwazi na kuwahamisha walimu kabla ya mwaka kukamilika ni vibaya sana maana walimu wanastahili kuhamishwa hadi shule zingine mwishoni mwa mwaka au mwanzo wa mwaka," alihoji Nyamwanda, mwenyekiti wa chama cha KNUT Nyamira.

Aidha, mwenyekiti huyo alidai kuwa baadhi ya walimu waliohamishwa hadi shule zingine ni wagonjwa na wengine ni wakongwe ambao wamezeeka jambo ambalo lilimpelekea kuomba mkurugenzi wa tume hiyo ya kuajiri walimu kusimamisha uhamisho huo.

"Tume hii ya TSC imeonekana kuenda kinyume na matarajio ya walimu wengine bila kujali maslahi ya wanafunzi au kuangalia umri wa walimu wakati wanafanya uhamisho huo," aliongeza Nyamwanda.

Sasa ni jukumu la tume hiyo ya TSC kusikia kilio cha walimu hao kupitia kwa mwenyekiti wao tawi la Nyamira kusimamisha uhamisho huo.