Maafisa wa polisi katika Kaunti ya Nyamira wamemtia mbaroni mwanamume mmoja anayehusishwa na kutupwa kwa mwili katika shamba moja lililoko eneo la Sotik Borabu siku ya Jumanne.
Kwa mujibu wa afisa mshirikishi wa Kaunti ya Nyamira Karimbo Mdohe aliyeongea na Waandishi wa habari siku ya Jumanne katika mji wa Nyamira, mshukiwa huyo kwa jina Joffrey Osanse na wengine wawili wanashukiwa kutupa mwili huo katika shamba hilo.
Washukiwa hao walikuwa na gari lao walipofika eneo la Ikonge ambapo maafisa wa trafiki waliwazuia, lakini wakatoroka na kufanikiwa kumtia mbaroni mmoja huyo baada ya kupashwa habari.
Afisa Mdohe alisema gari la washukiwa hao lililokuwa na rangi nyeupe aina ya Toyota kisu kilikuwa ndani pamoja na damu na baada ya uchunguzi kufanywa wakapata ni washukiwa hao walishukiwa kumuua na kutupa mwili huo.
Inasemekana kuwa marehemu aliuliwa katika Kaunti ya Kisii na mwili kusafirishwa hadi eneo la Sotik na kutupwa katika shamba hilo.
“Huenda mtu huyu aliuliwa katika Kaunti ya Kisii kisha mwili wake kusafirishwa hapa, lakini uchunguzi zaidi bado unaendelea kufanyika,” alisema afisa Mdohe.
Mwili wa marehemu ulihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Nyamira huku uchunguzi ukiendelea.