Maafisa wa polisi katika eneo la Kijauri, eneo bunge la Borabu, wameombwa kuhakikisha usalama wa kutosha ili kupunguza visa vya mauaji katika eneo hilo.
Wito huo umetolewa baada ya mwili wa kijana mmoja kupatikana katika mto wa kijauri siku ya Jumapili jioni ikiwa na majeraha.
Miili mingi ya watu imekuwa ikipatikana ikiwa na majeraha katika mto huo jambo ambalo limelazimu wakazi kuwaomba maafisa wa polisi kuhakikisha usalama wa kutosha katika mto huo ili kupunguza visa hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari siku Jumatatu mwenyekiti wa chama cha wakulima nchini, Patrick Osero aliwaomba maafisa wa polisi kuhakikisha usalama kwani wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakikabiliana na changamoto chungu nzima kama vile wizi wa ng’ombe na mauaji.
Osero alisema ikiwa washukiwa wa mauaji hao hawatachunguzwa na kutiwa mbaroni, basi washukiwa hao wataendelea kuwaua watu wengi na kuomba maafisa kuanzisha uchunguzi kubaini wanaotekeleza mauaji hayo.
“Naomba maafisa wa polisi kuweka usalama wa kutosha wakati wa usiku na mchana katika eneo hili ili tupunguze visa vya mauaji,” alisema Osero.
Kisa hicho cha kumpata kijana mmoja akiwa katika mto huo wa Kijauri siku ya Jumapili ni kisa cha tatu tangu miili mingine miwili kupatikana katika mto huo kwa wiki tatu zilizopita.