Mwenyekiti wa chama cha kupambana na dawa za kulevya nchini Nacada John Mututho ameomba machifu wote kutorudi nyuma katika zoezi la kumwaga pombe ambao ulianzishwa majuma matatu yalioyopita.
Akizungumza siku ya Jumatano katika eneo bunge la Nyaribari Chache alipokuwa na mkutano na machifu na maibu wao, Mututho alisema yeyote atakayerudi nyuma katika zoezi huo atakuwa akiweka kazi yake hatarini kwani pombe haramu haikubaliki kamwe nchini.
“Nataka kila chifu ahakikishe pombe haramu katika vijiji vyetu hapa Kisii imekomeshwa maana watu wengi wamepoteza maisha kwa kubugia pombe haramu. Hatuwezi kuangalia watu wakiendelea kupoteza maisha yao kiholela kwa kunywa pombe haramu,” alisema Mututho.
Aidha, Mututho alipongeza wale walioshiriki katika vita dhidi ya uuzaji wa pombe haramu kwa kumwagwa pombe hiyo katika sehemu mbalimbali za kaunti ya Kisii.
Wakati huo huo, Mututho alisema kuwa washukiwa wale wanaotiwa mbaroni wafikishwe mahakamani kujibu mashtaka ya kufanya biashara hiyo ambayo haikubaliki na serikali ya kitaifa.
Mututho pia aliwaomba wananchi wote kushirikiana pamoja kuendeleza umwagaji wa pombe haramu.