Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Madereva wa texi na haswa wale wa magari aina ya probox wameonywa dhidi ya kukiuka sheria za trafiki kwa kubeba abiria kupita kiasi.

Akizungumza ofisini mwake siku ya Jumatatu, Kamanda wa trafiki eneo la Kiambu Inspekta Gabriel Mulei alisema kwamba baadhi ya madereva wanabeba abiria wanaozidi wanne jambo ambalo halikubaliki.

Aidha, alisema baadhi ya madereva wa magari ya abiria yanayotumia barabara ya Kiambu wanasaidiana na wahudumu wa pikipiki kuwavukisha abiria wa ziada karibu na maeneo ambapo maafisa wa trafiki hukagua magari. 

"Abiria hao huabiri tena matatu hiyo hiyo baada ya kupita kizuizi cha polisi na kuendelea na safari yao," alisema Mulei.

Kamanda huyo wa trafiki amesema huenda idara hiyo italazimika kuwakataza waendeshaji wa bodaboda kusimama na kusubiri abiria katika eneo hilo ambapo wao husaidiana na wahudumu wa matatu kuvunja sheria. 

Inspekta Mulei alisema kuwa magari yote ambayo hayajatimiza kanuni zote za trafiki hayafai kuwa barabarani.

"Nimewaonya baadhi ya madereva wa magari na vile vile pikipiki ambao wamekuwa wakiwasafirisha abiria bila leseni na bima," alisema Mulei.

Inspekta huyo alisema kuwa maafisa wa trafiki hawatalegea wala kuendelea kuonya wale wanaovunja sheria za trafiki na kusema watakao patikana watafikishwa mahakamani. 

Aliuliza wahudumu wa matatu na wale wa magari ya probox kumaliza mzozo na badala yake kuheshimiana barabarani ili kupunguza ajali.