Shirika la ardhi la ‘Residents Land Protection Organisation of Kenya’ limeishinikiza serikali kubadili mbinu za kutatua mizozo ya ardhi nchini na hususan katika ukanda wa Pwani ili kuzuia kushuhudiwa kwa mizozo hiyo.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Mwenyekiti wa kitaifa wa Shirika hilo, Dewelly Nyambu, alisema kwamba tayari wanaharakati wa kutetea maswala ya ardhi nchini wamemuandikia barua Mwanasheria mkuu wa serikali Githu Muigai kuzishinikiza mahakama nchini kutatua mizozo ya ardhi mashinani badala ya kufanya vikao mahakamani.
Kulinagana na Dewelly, kesi za ardhi huchukua miaka mingi kutatuliwa kutokana na baadhi ya mawakili kukusanya stakabadhi nyingi kama ushahidi wa kutatua mizozo hiyo ilhali ushahidi kamili uko mashinani katika ardhi zenyewe.
“Tumemuandikia barua Githu Muigai ili atoe sheria ambayo italazimisha majaji kuzuru mashinani na kutatua kesi za mashamba kule mashinani maana mashahidi wale wa ukweli wako mashinani na ndio wanaojua mipaka kamili,” alisema Dewelly.
Dewelly pia amekashifu hatua ya waliyohusika katika uvunjaji nyumba za wakazi katika eneo la Dunga Unuse huko Changamwe mjini Mombasa, akisema kwamba hatua hiyo ni kuhujimu haki za Wakenya sambamba na katiba ya nchi jinsi inavyoangazia kuhusu maswala ya mizozo ya ardhi.
“Inasikitisha sana kuona maafisa wa utawala wakishirikiana na mabwanyenye kuwafurusha wakazi katika ardhi zao, mahali waliishi tangu jadi. Leo mtu anajitokeza na vyeti bandia vya ardhi watu wanafurushwa kwa kuwa hawajapata vyeti vya kumiliki ardhi,” aliongeza Dewelly.
Mapendekezo hayo yamejiri baada ya wakazi wa eneo la Pwani kulalamikia kudhulumiwa na baadhi ya mabwanyenye wanaoshirikiana na maafisa wa utawala ili kuwafurusha wakazi katika ardhi zao.