Mahakimu watatu wanaotumikia Idara ya Mahakama katika sehemu mbali mbali nchini wameachishwa kazi baada ya Bodi ya kuwakagua majaji na mahakimu kudhibitisha hawafai kutumikia idara hiyo.
Hata hivyo, wengine 23 waliidhinishwa na bodi hiyo wakati wa kutoa matokeo ya ukaguzi uliofanywa kwa muda wa miezi miwili. Walioachishwa kazi ni Teresia Njeri Ngugi, Bildad Ochieng na Lily Monica Nafula.
Huku akitoa matokeo hayo katika hoteli ya Masada mjini Naivasha siku ya Jumanne, mwenyekiti wa bodi hiyo Sharad Rao alisema shughuli ya kuwakagua mahakimu wengine 15 imeanza na itakuwa ya mwisho.
Bodi hiyo imeweka mipangilio ya kumaliza shughuli ya ukaguzi huo kabla ya tarehe 31 mwezi Machi mwaka ujao, wanapotarajiwa kung’atuka mamlakani.
"Maswala yaliyoibuka kwenye ukaguzi tuliofanya yalitegemea misingi ya uwezo wa mtu, ustadi, vitendo na uadilifu," alisema Rao.
Rao akiandamana na wanachama wa bodi hiyo, alisema Wakenya walitoa habari zilizoonyesha kuwa watatu hao hawakufaa kutumikia idara ya mahakama kwani maadili yao yanatiliwa shaka.
Mahakimu Thrispisa Wamae, Theresa Murugi, Paul Chepkonga, Doreen Nasieku, Heston Nyaga, Daniel Ogembo na Anne Colleta ni miongoni mwa wale waliodhinishwa kuendelea kutumikia idara hiyo.
"Hata hivyo, swala la jinsi wanaandikwa limeendelea kuwa tatizo katika kutoa huduma za mahakama,” alisema Rao.