Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Viongozi wote wa chama cha KNUT katika kaunti ya Kisii wamesema tume ya kuwajiri walimu nchini TSC haitawatisha kuwa itawasimamisha kazi ikiwa hawatarejea kazini.

Wito huo umetolewa baada ta tume hiyo ya TSC, kupitia mwenyekiti wa tume hiyo Lydia Nzomo, kutangaza kuwa itawasimamisha kazi walimu ambao wataendelea kugoma.

Wakizungumza na waandishi wa habari mnamo siku ya Jumanne katika mji wa Kisii, makatibu mbalimbali wa chama cha KNUT katika kaunti ya Kisii wakiongozwa na katibu Geofrey Mogire walikiri kuwa wamekuwa wakiheshimu uamuzi wa mahakama na kutaka serikali iheshimu uamuzi wa mahakama na kuwalipa walimu nyongeza yao ya mshahara.

“Walimu wataendelea kugoma na hatuwezi kutishwa kuwa tutafutwa kazi, tunahitaji haki yetu itendeke jinsi mahakama ilivyoamuru,” alisema Mogire.

“Tutarejea kazini ikiwa pesa zetu zimewekwa kwa benki zetu na hilo likifanyika basi hatuna lingine ila kurudi kazini,” aliongezea.

Wakati huo huo, katibu huyo alisema wakati huu ndio wakati wa kipekee walimu watalipwa pesa zao, na kuwapongeza wazazi kwa kushirikiana nao kuwatetea kulipwa pesa zao.

“Napongeza wazazi kwa kuweka watoto wao nyumbani na kushirikiana nasi ili tuongezewe mshahara. Naomba wazazi wote kuendelea kuomba serikali itulipe nyongeza yetu ya mshahara,” alihojoi Mogire.

Kulingana na katibu huyo, wako tayari kuendelea na mgomo hata kwa mwaka mmoja kuanzia sasa ikiwa hawatalipwa nyongeza yao ya mshahara.