Mbunge wa Mugirango Kusini Manson Nyamweya amewahakikishia wakaazi wa Kaunti ya Kisii kuwa atazipa kipao mbele barabara kwa kuziweka kuwa za lami iwapo atateuliwa kama gavana.
Mbunge huyo alikuwa akiongea katika eneo bunge lake baada ya kushiriki katika hafla ya kamati iliyoandaliwa na walimu wakuu wa shule za upili kujadili maendeleo na jinsi ya kuziendeleza shule zao kielimu, ambapo alihoji kuwa Kisii kama kaunti imefeli wakaazi kwa kutowajengea barabara za kudumu kuwafaa katika kusafirisha mali na bidhaa zao kutoka shambani kupeleka sokoni.
Alisema kuwa barabara za lami zitakuwa zenye manufaa makubwa kwa wakaazi wale wanaojihusisha na kilimo kama cha kufuga ng’ombe, cha mboga, matunda haswa ambao wakaazi wa eneo bunge lake wenye hutegemea kuchonga mawe na kuyasafirisha kwenda miji mikuu kama Nairobi lakini hukumbana na shida kutoa vinyago vya kutoka mashinani.
Nyamweya ambaye ametangaza nia ya kuwania kiti cha ugavana katika kaunti hiyo kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 alitoa mfano wa kaunti ya Machakos na Meru ambazo magavana wao wametumia pesa walizotengewa kwa kutengeza barabara za lami, jambo ambalo alisema gavana wa Kaunti ya Kisii hajafanya.
Alimtaka gavana wa Kisii James Ongwae kutia kichwa maji ili kujiandaa kupambana katika kipute cha kuwania ugavana mwaka wa 2017 kwani amejiandaa kutoana jasho kwenye uongozi wa kaunti hiyo awamu ijayo.