Mkewe gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae Elizabeth Ongwae ameahidi kuendelea kuwasaidia watoto wasichana katika kaunti hiyo kama njia moja ya kujiendeleza kimasomo.
Akiongea na wakazi wa Tabaka siku ya Jumanne katika uwanja wa shule ya Msingi ya Tabaka, eneo Bunge la Mugirango Kusini wakati aliwasaidia wasichana wa baadhi ya shule za msingi za eneo hilo na sodo kama njia moja ya kuhakikisha wasichana hao hawakosi shule wakiwa wanapata hedhi, bi Ongwae aliahadi kusaidia mtoto msichana ili kujiendeleza kimasomo na kuinua jamiii.
“Mtoto msichana katika jamii lazima asaidiwe ili aweze kujiendeza kimasomo kwani kuna changamoto nyingi ambazo wanapitia kwa hivyo weanastahili kusaidiwa, nami kama mama wao nitahakikisha wamesaidika kila wakati," alihoji bi Ongwae.
Aidha, alisema kuwa wao kama kaunti kupitia chama cha Lions Club, wataendelea kusaidia wasichana wote wa kaunti hiyo.
“Sisi kama Lions Club kutoka kaunti ya Kisii, tutahakikisha kuwa kila mtoto wa kike amesaidika naye aje kusaidia wenzake siku za usoni,” aliongeza bi Ongwae.
Kwingineko, aliwaomba wamama wote, haswa wasimamizi wa maendeleo ya wanawake kutoka Kaunti ya Kisii kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha wasichana hao wanasaidika kila wakati na kuwaonya wanaochukua fursa hiyo kujinufaisha wenyewe kwa kuuza sodo wanazopewa watoto hao wa kike kukoma tabia hiyo.