Share news tips with us here at Hivisasa

Mkutano wa kumuombea Naibu Rais Bw William Ruto na mwana habari Joshua Sang kuhusu kesi ambayo inawakabili katika mahakama ya kimataifa ya ICC umehairishwa..

Kuhairishwa kwa mkutano huo ambao ungefanyika katika Uwanja wa Huruma mjini Elodret siku ya Jumapili umeacha watu wengi na mshangao kwani maandalizi yote yalikuwa yamekamilika.

Waandalizi wa mkutano huo walisema kuwa kuhairishwa kwa mkutano huo kulitokana na kuwepo kwa mchuano wa soka katika uwanja huo siku ya mkutano husika.

Kwa mujibu wa mlezi wa muungano wa Jubilee North-Rift Bw Joseph Wainaina, mkutano huo umeratibiwa kufanyika Novemba 7 katika uwanja huo huo.

“Hatujahairisha mkutano huu kwa sababu za kisiasa, bali tumehairisha mkutano huu kutokana na kuwepo kwa mechi ya kandanda uwanjani humo wikendi hii,” alisema Bw Wainaina.

Bw Wainaina alisema mkutano wa tarehe saba utakuwa wa maombi ambapo waandalizi hawatakubali wanasiasa kutumia mkutano huo kuendeleza ajenda za kisiasa.

Kwa mujibu wa Bw Wainaina ni kwamba zaidi ya watu 20,000 kutoka kote nchini watahudhuria mkutano huo ambapo idadi kubwa ya watu hao watakuwa wahasiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007/2008.

Kumekuwa na tetesi kwamba viongozi wa kidini ambao wanapanga mkutano huo wamekuwa wakilumbana na baadhi ya wanasaisa ambao hawataki kutilia maanani maombi kama lengo kuu ya mkutano huo.