Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Afisa mmoja wa polisi, mlinzi wa benki ya Gulf Africa katika mtaa wa Bondeni mjini Mombasa, alipigwa risasi na genge la majambazi siku ya Ijumaa na kufariki papo hapo.

Kulingana na waliyoshuhudia kisa hicho, genge la majambazi waliyojihami kwa bunduki na bastola walienda katika benki hiyo na kuanza kuwafyatulia risasi maafisa wa polisi waliyokuwa wakishika doria katika lango la benki hiyo.

Akithibitisha kisa hicho, kamanda mkuu wa polisi katika Kaunti ya Mombasa, Francis Wanjohi, alisema kwamba afisa huyo wa polisi alipigwa risasi na kufariki papo hapo na genge hilo la majambazi lililofanikiwa kutoroka na bunduki ya afisa huyo aina ya G3.

“Afisa wetu mmoja wa polisi amepigwa risasi na majambizi alasiri ya leo na kumua papo hapo na wakatoroka na bunduki yake aina ya G3, aliyokuwa akishika nayo doria hapa kwa hii benki ya Gulf Africa. Tumeanzisha uchunguzi na tutawakabili washukiwa kisheria,” alisema Wanjohi.

Wanjohi alisema kwamba usalama umeimarishwa katika kaunti nzima ya Mombasa huku wakazi wakitahadharisha dhidi ya wahalifu wanaojitokeza na kutatiza usalama wa kaunti hiyo.

Mwili wa mwendazake umepelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali kuu ya ukanda wa Pwani huku uchunguzi ukianzishwa wa kulisaka genge hilo la majambazi.

Tukio hilo limejiri siku moja tu baada ya mfanyibiashara mmoja kupigwa risasi ya kichwa baada ya kukaidi kutoa pesa kwa genge la majambazi siku ya Alhamisi.