Naibu Gavana wa Mombasa Hazel Katana amesema kuwa wizara ya afya katika Kaunti ya Mombasa inapaswa kuajiri wauguzi wa afya 3,300 zaidi ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa.
Akizungumza siku ya Ijumaa kwenye kongamano la kujadili jinsi ya kuimarisha huduma za afya katika hiyo, Katana alisema kuwa Kaunti ya Mombasa ina wahudumu 1,537 pekee.
Alisema kuwa idadi hiyo ni ndogo mno kuweza kukidhi mahitaji ya watu wa Mombasa.
“Kiwango hiki ni kidogo mno na wauguzi 3,300 zaidi wanafaa kuajiriwa,” alisema Katana.
Naibu gavana huyo aliahidi kuwa serikali ya kaunti inajitahidi kuimarisha sekta ya afya ili huduma bora zitolewe kwa wakati ufahao.
Wakati huo huo, mwenyekiti wa kamati ya afya katika bunge la kaunti ya Mombasa Swaleh Baya alisema ipo haja ya wahudumu wa afya kupandishwa vyeo na mazingira ya kazi kuboreshwa kama walivyokuwa wakipendekeza wauguzi hao wakati wa mgomo.
Aidha, Baya alisema kuwa kuna uhaba wa wauguzi katika kaunti hiyo kwani kwasasa muhudumu mmoja anahudumia wagonjwa 50 jambo alililolitaja kama la kuhuzunisha.