Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Chama cha Green Firm Solution kwa ushrikiano na chama cha United States Agency for International Development (USAID) kimeanzisha mradi wa kupanda ndizi aina ya 'tissue culture' katika wadi zote 45 ziliomo Kaunti ya Kisii ili kuinua sekta ya kilimo na kuinua uchumi wa taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi mjini Kisii, msimamizi wa mradi huo wa upanzi Vick Onderi alisema wanahitaji kupanda ndizi millioni moja katika kaunti nzima ya Kisii ili kuimarisha uchumi wa taifa.

“Shule mbili zimechaguliwa kutoka kila wadi katika Kaunti ya Kisii ambapo tunaenda kufanya upanzi huu wetu wa ndizi mahala mtu anapata muda kufika na kununua na hata kushuhudia kilimo bora,” alisema Onderi.

Aliongeza “Kile ambacho kilitulazimu tufanye upanzi kwa mashule ni kuwa mashamba hayo ni ya serikali na yeyote anaweza kwenda na kushuhudia jinsi kilimo hufanywa bila kuogopa.”

Kulingana na Onderi, watu wawili kwa kila wadi watapata ajira ili kulinda ndizi hizo pamoja na miparachichi kama njia mojawapo ya njia ya kuzuia kuharibiwa kwa mmea huo.

Upanzi huo ulianzishwa katika wadi ya Nyacheki ambapo walifanya upanzi wa kwanza siku ya Alhamisi huku wakitarajia kuenda wadi zingine hadi wamalize.

Mwakilishi wa wadi ya Nyacheki, Peter Ongeri alipongeza mradi huo na kusema wengi watafaidika na upanzi huo kwa kupunguza hali ya umaskini katika kaunti ya Kisii.