Polisi katika eneo la Kikuyu wamemtia mbaroni mwanamume mmoja ambaye anadaiwa kuwalaghai wengi akitumia vyeti bandia kuwauzia shamba katika eneo la Ondiri.
Akidhibitisha kisa hicho siku ya Ijumaa, mkuu wa polisi katika eneo la Kikuyu Mutune Maweu alisema kwamba mshukiwa huyo amekuwa akiwindwa kwa kipindi cha miezi tisa sasa.
Alisema kwamba mshukiwa amedaiwa kuwalaghai watu zaidi ya sita pesa zao ambazo ukijumlisha ni Sh16m kwa kuwauzia shamba moja katika eneo la Ondiri ambalo si lake.
Maweu alisema kwamba mshukiwa huyo ambaye wengi wanamjua kama ‘broker’ ametumia mbinu hii ya ulaghai kuwahadaa wengi.
Alisema kwamba wakazi wa eneo la Zambezi ambao wamemjua kwa muda mrefu waliona vibango katika maeneo tofauti yaliyokuwa ya kumtafuta mshukiwa huyo.
Maweu alieleza kwamba mshukiwa alitiwa mbaroni nyumbani kwake kwa usaidizi wa majirani wake.
Polisi waliweza kupata vyeti bandia anazozitumia kutekeleza uovu huo.
Maweu aliwaonya wakazi dhidi ya kununua ardhi bila kuhusisha wizara ya ardhi kwa kuwa walaghai wa aina hiyo ni wengi.
"Kwa wale ambao wanatekeleza uovu huu, siku zao zinakaribia. Wakazi pia nawaonya dhidi ya kukimbilia biashara za aina hii kabla ya kufikiria athari zake," alisema Maweu.
Hata hivyo, aliwapongeza wakazi waliorepoti kuhusu mshukiwa na kuwahimiza wakazi wawe na ukaribu na mawasiliano na polisi ili kuimarisha usalama na utulivu.
Alisema mshukiwa amezuiliwa katika Kituo cha polisi cha Kikuyu akikabiliwa na mashtaka ya ulaghai na atafikishwa mahakamani siku ya Jumatatu.