Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa jumuia ya magavana kutoka Pwani amewataka magavana wenzake kuacha ubinafsi na kushikana pamoja ili kuwezesha kuimarika kwa uchumi wa kaunti sita za eneo la pwani.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni gavana wa kaunti ya Kwale, Bwana Salim Mvurya, alisikitikia jinsi viongozi wa kaunti wanavyochukulia mshikamano wao kwa njia ya kisiasa.

Mvurya alidai kuwa baadhi ya magavana wa kaunti zingine hawataki kuleta maendeleo kwa maeneo ya pwani na wana ajenda za binafsi huku akiwataka wananchi kuwaangalia kwa jicho la ndani wanaporudi kuomba kura katika uchaguzi mkuu ujao.

Akiongea katika kongamano lililowaleta pamoja wataalam mbalimbali pamoja na washikadau katika masuala ya biashara siku ya Alhamisi katika eneo la Diani, Mvurya alisema kuwa ni wakati wa viongozi kutoka eneo zima la pwani kuja pamoja na kuwafaidi wakazi ili kusukuma ajenda moja ya maendeleo.

Kongamano hilo lililenga kuwaleta pamoja magavana sita kutoka kaunti za Lamu, Kwale, Mombasa, Kilifi, Taita Taveta pamoja na Tana River kuweka mawazo pamoja ya kuboresha na kuimarisha uchumi kwenye kaunti hizo lakini hakuna gavana alijiyetokeza kwenye mkutano huo ila Salim Mvurya ambaye pia ndiye alikuwa mwandalizi mkuu wa hafla hiyo.