Mwakilishi wa wadi ya Sensi iliyoko eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini, Ochong’a Nyagaka amesema atafungua soko mpya katika eneo la Sensi ili wafanyi biashara waweze kuinua uchumi wao kupitia biashara.
Hii ni baada ya wakazi wa eneo hilo kuomba mwakilishi huyo kuwafungulia soko mpya katika eneo hilo kwani wakazi hao walisema wanatembea kilomita nyingi ili waweze kufika katika soko la eneo la Marani, jambo ambalo waliwasilisha kwa mwakilishi wao.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumapili katika mji wa Kisii, mwakilishi huyo alisema mikakati ya kufungua soko hiyo imeimarishwa kikamilifu na soko hiyo itafunguliwa wakati wowote kuanzia sasa.
“Wakaazi wa eneo langu waliniomba niwafungulie soko mpya katika eneo la Sensi. Tayari mikakati imeimarishwa na nitafungua soko hilo hivi karibuni,”alisema Nyagaka.
Aliongeza: “Tunahitaji kupunguza umaskini katika jamii yetu ya wakisii kwa kufanya biashara na tunahitaji kuinua uchumi katika kaunti yetu ya Kisii kupitia biashara."
Wakati huo huo, mwakilishi huyo aliomba akina mama wote katika wadi yake kujiunga pamoja na kuunda vikundi ili wapate pesa za mikopo ili waweze kufanya biashara kama njia moja ya kuinua uchumi wa kaunti.
“Naomba akina mama wote hasa wafanyi biashara wazipe biashara zoa kipau mbele maana kupitia biashara, kaunti yetu itainuka zaidi,” alisema Nyagaka.