Mwakilishi wa wadi ya Bonyamatuta Robinson Mocheche amesema maafisa wanne walioondolewa madai ya ufisadi warudi mamlakani na kufanya kazi jinsi waliovyokuwa wanafanya hapo mbeleni.
Hii ni baada ya wawakilishi wa Kaunti ya Nyamira kukataa kupitisha ripoti ya jopo lililoundwa kuwachunguza maafisa waliohusishwa na sakata ya ufisadi ambayo ilisema kati ya maafisa hao sita, ni wawili tu waliohusishwa na ufisadi.
Akizungumza siku ya Jumanne katika makao ya bunge la Kaunti ya Nyamira, mwakilishi huyo alisema wale walioondolewa madai hayo waanze kufanya kazi yao kama kawaida maana hakuna ushahidi wa kuonyesha kuwa walijihusisha na ufisadi.
Maafisa walioondolewa madai ya kujihusisha na sakata hiyo ya ufisadi kulingana na ripoti hiyo iliyosomwa na mwenyekiti wa jopo lilioundwa kwachunguza maafisa hao ni Mkuu wa Idara ya Barabara Kepha Osoro, Mkuu wa Idara ya Maji Andrew Ombati, Fridah Nyaboga na Morara Mokua.
“Mimi ninaona kuna wawakilishi wa kaunti hii ambao ni vibaraka na hawataki serikali yetu iendelee mbele. Naomba wale waliondolewa madai ya ufisadi warejelee kazi yao jinsi walikuwa wanaifanya,” alisema Mocheche.
Maafisa waliohusishwa na ufisadi huo ni Mkuu wa Idara ya Michezo na Utamaduni Peter Omwanza na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Fedha John Omanwa.