Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mama mwenye umri wa miaka arobaini, alinusurika kifo siku ya Jumanne baada ya kupigwa na wakazi wa eneo la Jogoo kwa kushukiwa kumroga msichana mwenye umri wa miaka kumi na miwili.

Wakazi kutoka eneo la Nyankongo, KARI pamoja na Jogoo walitaka kumuua mama huyo na ilibidi maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Jogoo kuingilia kati na kumuokoa mama huyo.

Samuel Moi, ambaye alishuhudia kisa hicho, alisema kuwa kuna madai kuwa mtoto huyo ambaye ni wadarasa la sita katika shule ya msingi ya Jogoo, alitolewa kwenye chumba anacholala na zaidi ya watu kumi ambao walimbeba na kumtembeza usiku na baadaye kumrudisha nyumbani asubuhi ya Jumanne akiwa hazungumzi.

Moi alisema kuwa msichana huyo hakuwa na uwezo wa kuongea na ikambidi mama ya msichana huyo kutafuta nguvu za maombi.

Inadaiwa kuwa katika harakati za kuenda kumwona mhubiri mmoja katika eneo hilo, ndipo mwaathiriwa alipoweza kumtambua mama huyo mshukiwa wa uchawi.

Kulingana na mila za Wakisii, mshukiwa wa uchawi anahitajika kumtemea mate mwaathiriwa kitu ambacho mama huyo aliweza kufanya.

Inasemekana kuwa pindi tu baada ya mama huyo kumtemea msichana huyo mate, aliweza kuanza kuongea na kumtambua mama huyo.

Dennis Omwansa, aliyeshuhudia kisa hicho, alisema hapo ndipo wakazi walianza kumvamia ambapo maafisa wa polisi kutoka Idara ya Utawala waliweza kuingilia kati kwa haraka na kumuokoa kabla ya kuchomwa na wakazi hao ambao walikuwa na hasira.

Hata hivyo, mshukiwa huyo aliweza kuondolewa kwenye kambi hiyo na kupelekwa hadi kituo cha polisi cha Kisii Central, huku polisi wakiendelea kupiga doria kuwazuia wakazi dhidi ya kuenda kuchoma nyumba yake.

Polisi walisema kuwa uchunguzi umeanzishwa kuhusiana na kisa hicho.