Mwanamume wa umri wa makamo allipoteza maisha yake baada ya kupigwa na nguvu za umeme na kufariki papo hapo mjini Kisii siku ya Jumatano jioni.
Akitibithisha kisa hicho, mkuu wa polisi wilayani Kisii ya kati Francis Nguri alisema mwanamume huyo aliaga dunia baada ya nyaya za stima kukatika na kumwangukia, alipokuwa anakimbia kujikinga na mvua nyuma ya jengo la duka la jumla la Tuskys.
Ajali hiyo ilisababishwa kupitia mvua nyingi iliyoshuhudiwa katika eneo hilo, ambayo ilikuwa na upepo mkali na kupelekea kuangusha nyaya za stima na kugharimu maisha ya jamaa huyo.
Wakazi wengi mjini Kisii wamelaumu kampuni ya umeme nchini KPLC kwa kutoweka nyaya hizo inavyostahili, na kupelekea kukatika.
Mwili wa marehemu ulipelekwa hadi chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Kisii, huku uchunguzi ukiendelea kufanywa kubaini mwanamume huyo anatoka sehemu gani.
Hii si mara ya kwanza nguvu za umeme kugharimu maisha ya watu katika kaunti ya Kisii, na inaleta hofu miongoni mwa wakazi.
Ikumbukwe kuwa siku ya Jumamosi, mwanamume mwingine kutoka eneo la kiogoro alifariki baada ya kupigwa na nguvu za umeme na kufariki papo hapo.