Naibu polisi mkuu wa eneo la Nyankanga eneo bunge la Bonchari, amewahakikishia machifu kuwa wataendelea kushirikiana katika shughuli ya kumaliza pombe haramu.
Hii ni baada ya baadhi ya machifu na manaibu wao kutoka eneo hilo kulalamika kuhusu ukosefu wa ushirikiano kati yao na maafisa wa polisi, katika harakati za kudhibiti unywaji pombe na matumizi ya dawa za kulevya.
Machifu hao walisema kuwa baadhi ya maafisa wa polisi wamekuwa wakiwanyanyasa wanapowashika wagemaji na wanyuaji.
Akiwahutubia waandishi wa habari katika mji wa Suneka siku ya Jumatano, Naibu polisi mkuu Bwana Tom Onderi alisema kuwa tayari ameyasikia malalamiko ya machifu hao pamoja na manaibu wao na atahakikisha kuwa uhusiano uliopo kati ya maafisa wa polisi na wao unadumishwa kwa umuhimu wa kuifaa jamii kwa jumla.
Onderi aliwataka machifu hao pamoja na manaibu wasitishiwe na yeyote na kusema kuwa miongoni mwa jamii kuna watu ambao hawapendi kuona mabadiliko na msako kama huo umewaathiri wengi.
“Tuwe wakakamavu kupigana na matumizi na unywaji wa pombe haramu. Madai yenu yatafanyiwa uchunguzi ili kuleta uwiano miongoni mwenu,” alisema afisa huyo.
Aidha, afisaa huyo aliwaomba machifu wasirudi nyuma huku akisema kuwa madai hayo yataangaliwa na uchunguzi kufanywa ili kubaini ni nani anazuia juhudi hizo za serikali.
Msako wa pombe haramu umekuwa ukiendelea kwa wiki tatu sasa kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta ambaye aliwataka maafisa wa utawala kuanzisha operesheni ya kupunguza ulevi na ugemaji wa vileo nchini.