Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir amewashauri wazazi wa walioathirika na utumizi wa dawa za kulevya kutowatenga vijana, bali kuwasaidia kujikwamua kutoka kwa janga hilo.
Akizungumza siku ya Jumapili katika kituo cha kurekebisha walioathirika na dawa za kulevya cha 'Reachout' huko Likoni, mbunge huyo alisema kuwa licha ya wao kupokea matibabu na kubadili mienendo yao, jamii bado inawanyanyapaa kiasi cha kuwafanya kurudia mihadarati.
Maneno yake yaliungwa mkono na mkurugenzi wa kituo hicho Taib Abdulrahman, ambaye aliwataka waraibu kujizatiti kujitoa katika uraibu huo kwa sababu matibabu inategemea kujitolea kwao.
Vijana hao wanaoendelea kupokea matibabu wamewataka wenzao ambao bado wanaendelea kutumia mihadarati kujitokeza kusaidiwa ili kujenga maisha yao.