Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Asilimia 90 ya vijana wanaojiunga na makundi haramu ya kigaidi ni wanafunzi kutoka vyuo vikuu humu nchini.

Akiongea katika halfa ya kuwahamisha vijana jinsi ya kuepukana na makundi ya kigaidi kama lile la Al-shabaab katika chuo kikuu cha Nairobi tawi la Mombasa siku ya Jumanne, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nasir alisema kwamba kuna haja ya shule za msingi, upili na vyuo vikuu kuanzisha vipindi vya hamasa kusuhu jinsi vijana wa shule wanaweza kuepukana na makundi ya kihalifu na misimamo mikali.

Nassir amewahimizi walimu katika shule hizo na vyuo vikuu mjini Mombasa kutoa mafunzo yatakayowasaidia vijana kujikinga na vishawishi vibaya kutoka kwa watu binafsi waliyona malengo ya kuvuruga ndoto za vijana katika siku za usoni.

“Kuna haja ya walimu kubuni vitengo maalum vya kutoa mafunzo kwa wanafunzi jinsi ya kuepukana na kujiunga na makundi ya kihalifu ili kudumisha usalama wa nchi,” alisema Nassir.

Nassir aidha amewataka wazazi kuwashauri vijana wao sawia na kujitokeza kushirikiana na serikali pamoja na maafisa wa polisi katika kutatua tatizo hilo ili kuona kwamba vijana wananusurika na ugaidi na maswala ya misimamo mikali.

“Ni lazima kwa wazazi kuwashauri vijana wao kuzingatia maisha yao katika siku za usoni kwani hatua hiyo itasaidia pakubwa kudhibiti usalama na kuwazuia vijana wetu kujiunga na makundi ya kigaidi kwa asilimia kubwa ya vijana hutoka katika vyuo vikuu,” aliongeza Nassir.

Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa chuo kikuu cha Nairobi tawi la Mombasa Josephat Mali aliunga mkono kauli ya mbunge huyo wa Mvita akisema kwamba tayari chuo hicho kina mpango wa kuanzisha kitabu cha kuwasaidia wanafunzi kuhamasishwa kujitenga na makundi ya kigaidi na maswala ya misimamo mikali.

Haya yamejiri huku swala la misimamo mikali na ugaidi likikithiri katika eneo zima la Pwani.