Huku vijana wakionekana kupotoka na kutumia wakati wao mwingi kwenye safu za mitandao, wamepewa changamoto kuanza kukumbatia mtindo wa kusoma vitabu vya fasihi ili kujikomaza zaidi katika masomo.
Akihutubia zaidi ya washiriki elfu mbili waliokongamana kwenye ukumbi wa maktaba makuu ya chuo kikuu cha Kisii siku ya Jumatatu, msomi maarufu ambaye pia ni mwandishi wa vitabu Prof Ngugi wa Thiong'o, alisikitikia hali na mienendo miongoni mwa vijana ambao wanaonekana kuegemea sana uandishi wa mkato ambao hutumika sana na watumizi wa vitandawizi.
Profesa Thiong'o alionya kuwa iwapo vijana hawataelekezwa vizuri na kujiepusha dhidi ya mwelekeo huo ambao wamechukua, huenda kukakosekana kabisa waandishi wa vitabu katika siku zijazo.
Mwandishi huyo wa vitabu maarufu ambavyo baadhi yao hutahiniwa rasmi kwenye shule za upili nchini, aliwashauri wanafunzi kutoka chuo hicho pamoja wa wasomi waliokuwa kwenye hafla hiyo kutenga muda angaa saa moja kila siku ili kuvisoma vitabu kama njia mojawapo ya kujinoa maarifa.
“Naomba jumuia ya wanafunzi pamoja na wakenya kwa jumla kuwa katika mstari wa mbele kwenye masuala ya masomo,” alisema Thiong'o.
Hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na kiongozi wa mlengo wa upinzani Cord Bwana Raila Odinga, pamoja na viongozi tofauti kutoka serikali ya kaunti ya Kisii, ulishuhudia kufana kwa hafla hiyo huku wengi wa wakazi kutoka Kisii wakifurahia kumwona mwandishi huyo kwa mara ya kwanza.