Chifu wa Lokesheni wa Mochenwa, Wadi ya Gesima ilioko eneo Bunge la Kitutu Masaba amesema hatakubali kupoteza kazi yake kwa ajili ya kuruhusu pombe haramu katika lokesheni hiyo.
Akiongea siku ya Jumatatu katika ofisi yake na manaibu wake pamoja na wazee wa vijiji katika Ritongo, Wadi ya Gesima katika Kaunti ya Nyamira, chifu Magara Makori alisema kuwa yeye hatakubali kamwe kupoteza kazi yake kwa kuwaruhusu wagema katika lokesheni yake kuendelea na biashara hiyo ambayo imepigwa marufuku kufuatia vifo vya watu wanaokunywa pombe hiyo, bali ni wagema watalazimika kuacha upikaji wa pombe hiyo.
“Kutokana na agizo la Raisi Uhuru Kenyatta wiki iliyopita nitahakikisha kuwa biashara ya pombe imeisha katika lokesheni yangu maanake sitaki kulaumiwa kwamba sijawajibika kazini kwa hivyo ni tahadhari kwa wagema wote kuwa wakati wao umeisha na biashara ya kuhatarisha maisha ya watu kwa kuwauzia pombe haramu katika lokesheni yangu haina nafsi tena,” alihoji chifu Makori.
Aidha, chifu huyo aliwaomba manaibu wake Richarad Makworo na Simeon kuwajibika kazini kwa kushirikiana na wazee wa vijiji ili kuhakikisha biashara ya pombe hiyo imeisha.
Chifu Makori alisema wakazi nao wanastahili kuunga mkono msako wa pombe haramu kwa kuacha kuwalaumu wanaofanya shughuli hiyo ya msako kwa kusema kuwa pombe imesaidia familia nyingine kuwasomesha wanao na kuongeza kuwa mambo hayo yamepitwa na wakati.
Wakazi hao kwa sasa wameombwa kushirikiana na maafisa wa Polisi na kuripoti mahali kuna pombe hiyo haramu ili wagema waweze kufikiwa na kuchukuliwa hatua ya kisheria.