Share news tips with us here at Hivisasa

Seneta wa Kaunti ya Mombasa ametetea chama cha Wiper kwa kusema kuwa chama hicho kiko imara na wale ambao wanajaribu kukivunja hawatafua dafu kamwe.

Akiongea katika mji wa Mombasa siku ya Jumapili, Hassan Omar alisema kuwa wakati wa siasa bado haujafika na wale ambao wanaendelea kujaribu kuleta mgongano katika chama hicho wanania ya kuwatenganisha viongozi wa chama hicho.

Alisema kuwa Wiper pamoja na chama cha ODM na muungano wa Cord kwa jumla wanaendelea kuimarika kila kukicha na kuwataka wafuasi wao kubaki imara hadi uchaguzi mkuu ujao.

Seneta huyo aliwaomba viongozi wa vyama vyote ambavyo vinaunda muungano huo kuwa na imani kwenye muungano huo na kuacha kutumiwa vibaya na wanasisa wengine ambao wana nia mbaya.

“Wale ambao wanadhani kuwa watatutenganisha watangoja kuona hayo kwani chama chetu na muungano wetu kwa jumla utaendelea kuwa imara kuliko wanavyodhania. Wale ambao wanatuunga mkono nawaomba wabaki kutuunga siku zote,” alisema Omar.

Haya yanajiri baada ya baadhi ya viongozi wengi kutoka chama hicho cha Wiper kuonekana kugawanyika kwa pande mbili.