Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae amekiri kuwa hajaridhika na jinsi maendeleo yalivyofanywa katika kaunti hiyo na kuahidi kuwa atahakikisha kuwa ameleta maendeleo zaidi.

Akizungumza siku ya Alhamisi katika uwanja wa michezo wa Gusii, Ongwae alisema hajaridhika na utendakazi wa serikali yake, haswa yale aliyowaahidi wananchi wakati wa kampeini na kusema atatekeleza ahadi zote kikamilifu.

Ongwae alisema maendeleo mengi hayajakamilika kwani pesa zinachelewa kutumwa kwa kaunti na kuwataka maafisa wake wa kaunti kufanya maendeleo zaidi pindi pesa zinapofika kwa kaunti kila mwaka ili kuafikia matarajio yake kwa maendeleo kabla ya uchaguzi ujao.

“Sijaridhika na kiwango cha maendeleo katika kaunti yangu ila nitashirikiana na maafisa wangu ili tuhakikishe maendeleo niliyowaahidi wananchi wa kaunti nzima yametimizwa kikamilifu,” alisema Gavana Ongwae.

Kulingana na matokeo yaliyotolewa kwa miezi michache iliyopita, kaunti ya Kisii iliorodheshwa kuwa ya nne kwa maendeleo kote nchini huku Ongwae akisema serikali yake itajaribu kila iwezalo kuhakikisha imefanya mengi zaidi katika maendeleo.

Wakazi waliohudhuria hafla hiyo walisema wamefurahishwa na maendeleo yaliyoletwa katika kaunti hiyo, haswa ukarabati wa baadhi ya barabara, kuweka taa katika masoko na ukarabati wa baadhi ya chemichemi za maji.

Ongwae aliahidi kuwa kila mwaka atatengeneza barabara kilomita 500 ili kuimarisha sekta ya uchukuzi katika kaunti hiyo.