Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kisii ameahidi kuongeza hela za elimu kutoka Sh3m hadi Sh5m katika kila eneo la uwakilishi wadi.

Gavana Ongwae alisema kuwa atajitahidi kwa kila awezalo ili kuona kila mtoto kutoka kaunti ya Kisii anapata elimu, na kila shule inafaidi kutokana na hela hizo ambazo zimewekwa mahususi kwa masuala ya ufadhili wa wanafunzi kielimu.

Akiwahutubia viongozi wa vyama vya kutetea haki za walimu kutoka Kaunti ya Kisii kwenye ofisi yake siku ya Alhamisi, Ongwae aliwaambia walimu hao kuwa hela hizo zitakuwa zinaenda moja kwa moja hadi shule na kuwafadhili wanafunzi husika na kuwataka walimu hao kutoa mwongozo katika matumizi ya hela hizo.

Viongozi wa vyama hivyo ambavyo vilijumuisha chama cha Knut na chama cha Kuppet, walitaka kujua msimamo wa Gavana James Ongwae kuhusiana na mgomo wa walimu ambao unaendelea kote nchini.

Hata hivyo, Gavana Ongwae aliweza kuwapa matumaini kwa kuwaambia kuwa yupo nyuma ya mgomo wao na iwapo walimu watafuata mkondo wa kisheria kuwasilisha matakwa yao kwenye tume ya kuwaajiri walimu nchini, pamoja na wizara husika, basi ataendelea kuwaunga mkono.

“Mimi kama gavana niko nyuma yenu lakini sharti mfuate njia ambayo inakubalika kisheria na kuwasilisha kilio chenu kisheria,” alisema Ongwae.