Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae amemuomba mkurugenzi mkuu wa kampuni ya nguvu za umeme nchini, Ben Chumo kujadiliana na Rais Uhuru Kenyatta ili kupunguza gharama ya kuunganisha umeme.

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa ingawa gharama hiyo ya pesa ilipunguzwa kutoka Sh35,000 mpaka Sh15,000 bado kuna baadhi ya wananchi ambao hawana uwezo wa kupata pesa hizo.

Akiongea siku ya Alhamisi katika hafla ya uzinduzi wa ofisi mpya ya Kenya Power ya mkoa wa Nyanza kusini, katika ofisi ya kampuni hiyo ilioko mjini Kisii, Ongwae aliomba gharama hiyo kuendelea kupunguzwa kwani wengi wanahitaji nguvu hizo za umeme lakini hawana uwezo.

‘Naomba gharama hiyo ya Sh15,000 ambazo mwananchi anastahili kuwa nazo ili kuunganishiwa nguvu za umeme iweze kupunguzwa hadi Sh10,000 ili kila mtu aweze kunufaika,” alisema Gavana Ongwae.

Aliongezea “Naomba ujadili na Rais Kenyatta ili gharama hiyo muweze kuipunguza tena kutoka mahala iliyoko kwa sasa.”

Mkurugezi huyo, Ben Chumo alisema kufikia sasa watu 87,000 wameunganishiwa nguvu za umeme mkoani Nyanza Kusini

Ofisi hiyo ambayo ilifunguliwa itahudumia kaunti nne zikiwemo kaunti ya Kisii, Nyamira, Migori na Homabay.

Aidha, chumo aliomba kila mtu kuhakikisha anatumia nguvu za umeme ili kuinua uchumi katika taifa la Kenya.